Ligi ya mabingwa sare zatawala ufunguzi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mlinzi wa Chelsea Gary Cahill mwenye jezi ya njano akikabiliana na mshambuliaji wa Paris Saint Germain ya Ufaransa Zlatan Ibrahimovic. Timu hizo zilifungana 1-1

Michezo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, UEFA ilianza kutimua tena vumbi Jumanne usiku kwa michezo miwili katika hatua ya kumi na sita bora.

Paris Saint Germain ya Ufaransa iliwaalika Chelsea ya England, huku Bayern Munich ya Ujerumani wakiwa wageni wa Shaktar Donetsk ya Ukraine. Matokeo ni kwamba PSG na Chelsea zimemaliza dakika tisini za mchezo kwa kufungana bao 1-1.

Chelsea ndio waliokuwa wa kwanza kutikisa nyavu za wenyeji wao katika dakika ya 36, bao likifungwa na Branislav Ivanovic na kudumu hadi mapumziko. PSG waliendeleza mashambulizi huku kiungo wake David Luiz akiwadhibiti wachezaji wa timu yake ya zamani, Chelsea. Kwa David Luiz kutawala sehemu ya kiungo, mshambuliaji Matuidi wa PSG alikuwa akitamba na kuelekeza mashambulizi makali langoni mwa Chelsea na kumfanya mlinda mlango wake Curtois kuokoa michomo mingi. Katika dakika ya 54 ya mchezo, Edinson Cavani aliisawazishia timu yake bao na hivyo hadi mwamuzi anapuliza filimbi yake ya mwisho, timu hizo zilitoka sare ya bao1-1.

Image caption Bayern Munich ya Ujerumani katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora walipomenyana na Shakhtar Donetsk na kutoka sare ya 0-0

Nayo Bayern Munich ya Ujerumani ilishuhudia ikitoka sare ya kutofungana na Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Bayern Munich ilipata pigo kwa mchezaji wake Xabi Alonso kuzawadiwa kadi nyekundu katika mchezo uliojaa ubabe.

Jumatano usiku, Real Madrid ya Hispania watakuwa wageni wa Schalke 04 ya Ujerumani katika mchezo mwingine wa klabu bingwa, huku Basel ya Uswis ikiikaribisha FC Porto ya Ureno.

Mechi za hatua ya kumi na sita bora zitakamilika Machi 18, ambapo michezo miwili miwili itakuwa ikifanyika Jumanne na Jumatano.

Timu nyingine katika hatua hii ni Juventus ya Italia itakayopambana na Borussia Dortmund ya Ujerumani, Manchester City ya England itavaana na Barcelona ya Hispania, mechi zitakazochezwa usiku wa tarehe 24 Februari na kesho yake yaani tarehe 25 Februari Arsenal ya England itakuwa ikipimana misuli na Monaco ya Ufaransa, huku Bayern Levkusen ya Ujerumani wakiwa wenyeji wa Atletico Madrid ya Hispania.