Mapigano yazuka tena Ukraine

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mwanajeshi wa Ukraine akilielekeza uelekeo gari la jeshi

Mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya Ukraine na Waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa mji wa Debaltseve, japokuwa kuna makubaliano yanayo taka makundi hayo kusimamisha mapigano. Taarifa za mitandao ya kijamii pamoja na matangazo kutoka kwa afisa mwandamizi wa jeshi la Ukraine Semen Semenchenko, zinasema kuwa vikosi vya Ukraine vinasukumwa nje ya mji huo muhimu. Lakini katika mahojiano yaliyofanywa na BBC na balozi wa Ukraine katika umoja wa nchi za Ulaya Kostiantyn Yelisieiev amekanusha kwamba vikosi vya nchi hiyo vimerudisha nyuma. Balozi huyo ameomba msukumo zaidi kimataifa kwa nchi ya Urusi kuzuia waasi kuendelea kupambana. Awali makamu wa rais wa Marekani Joe Biden aliionya Urusi juu ya hasara inayopatikana kama inaendelea kukiuka mkataba wa kusimamisha mapigano.