Obama:Vita ni dhidi ya magaidi si Uislam

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama ameliambia kongamano dhidi ya misimamo mikali ya kidini akisema kuwa kuwa wako kwenye vita si na Waislamu bali na magaidi waliouchafua Uislamu.

Bwana Obama amesema ni sharti dunia ikabiliane na itikadi zilizopindishwa na makundi kama Islamic State yanayochochea vita na kuwapa vijana mafundisho yenye misimamo mikali ya imani ya kidini .

Ameyasema hayo katika mkutano wa siku tatu unaofanyika mjini Washington ambapo amesema dunia inatakiwa kukabiliana na makundi ya aina hiyo.

Rais Obama ameeleza kuwa manung'uniko waliyonayo vijana lazima yashughulikiwe ili kuondokana na hisia za makundi yenye misimamo mikali ya kiitikadi.

Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi sitini wanahudhuria mkutano huo ambao umekuja kufuatia mashambulio ya makundi ya Kiislam katika nchi za Denmark, Ufaransa na Australia.