Burundi,Kenya zafuzu wavu kanda ya Tano

Image caption Bendera ya taifa ya Burundi

Timu za taifa za mpira wa wavu za Burundi na Kenya zimefuzu kutoka kanda ya tano ya Afrika ya michezo ya wavu ya ufukweni ambapo sasa itawania kucheza michezo ya Olimpiki ya michezo hiyo itakayofanyika mwaka kesho mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Timu ya Burundi ya wanaume zimeibuka washindi kwa kupata pointi 15 huku Kenya ikipata pointi 12 na Tanzania kuambulia pointi tisa. Na kwa upande wa wanawake Kenya imepata pointi 15 wakifuatiwa na Burundi yenye pointi 12 na Tanzania kupata pointi tisa.

Michuano hii ya kusaka wawakilishi kutoka kanda ya tano ilizishirikisha timu tatu za Burundi, Kenya na Tanzania wenyeji baada ya timu za Ethiopia, Djibouti na Somalia kushindwa kushiriki tangu akuanza kwa michuano hiyo Februari 16.

Kwa matokeo hayo timu za Burundi na Kenya zitapambana na timu kutoka kanda nyingine za Afrika mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo baadaye mwaka huu ili kupata timu za mpira wa wavu wa ufukweni zitakazoiwakilisha Afrika katika michuano ya Olimpiki ya Rio de Janeiro nchini Brazil mwakani.