Wapenzi wa jinsia moja washtakiwa Kenya

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wapenzi wa jinsia moja

Wanaume wawili katika eneo la Kwale Pwani ya Kenya wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.

Wawili hao wamekamatwa wiki moja tu baada ya polisi kudokeza kuwa wanachunguza watalii wanaohusika na utengenezaji wa video za ngono katika Pwani ya Kenya.

Watu hao walifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa Kwale, wakikabiliwa na shtaka la kushiriki katika ushoga kinyume na sharia za nchi.

Mashtaka yalieleza kuwa washukiwa, wakiwa wanaume, walifanya mapenzi baina yao wawili.

Lakini hawakuhitajika kujibu mashtaka, huku Polisi wakiomba muda zaidi kuchunguza uwezekano wa watalii kuhusika katika jambo hilo.

Vilevile kiongozi wa mashtaka aliiambia mahakama kuwa washukiwa walikataa kufanyiwa ukaguzi na madaktari . Washukiwa nao walilalamika kuwa polisi wamewahangaisha na kuwapiga.

Hakimu aliamrisha wazuiliwe hadi tarehe 24 Februari watakapohitajika kujibu mashtaka.

Aidha aliamuru wakubali kufanyiwa ukaguzi na daktari. Wiki iliyopita mamlaka ya Kwale iliambia waandishi wa habari kuwa Polisi walikuwa wakiwachuguza watalii fulani wanaoshukiwa kusimamia na kueneza kanda za video za ngono.

Ni habari ambayo imewakera wenyeji wengi wa maeneo ya Diani na Ukunda, wakilalamikia kuchafuka kwa jina lao na maadili yao.

Watalii wanaosakwa wanaaminika kuwalipa wenyeji kufanya mapenzi ya jinsia moja, pamoja na ngono kwa watoto.