Hatimaye Simone Gbagbo afikishwa mahakani

Haki miliki ya picha
Image caption Mke wa Rais wa zamani, Laurent Gbagbo Simone.

Mke wa Rais wa zamani, Laurent Gbagbo, anayekabiliwa na kesi inayohusiana na makosa ya ukiukaji wa haki za kibinadamu

katika mahakama ya kimataifa ya Jinai, ICC mjini Hague, anashtakiwa pamoja na wakuu wengine katika serikali yake katika mji wa Abidjan

kwa kuchangia pakubwa ghasia zilizozuka baada ya Bwana Gbagbo kukataa matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanywa Desemba 2010.

Kulingana na mashtaka yanayomkabili mke wa Gbagbo na washtakiwa wenzake, walitumia wapiganaji wa kiraia wakatili kuwashambulia

wafuasi wa mshindi wa Uchaguzi huo, Rais Alassane Ouattara, ingawa wafuasi wake pia wanadaiwa kutekeleza ukatili ambao kwa ujumla ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.

Gbagbo na mkewe walitiwa mbaroni Aprili 2011, ambapo Simone, alizuiwa katika jela moja Kaskazini mwa taifa hilo la Magharibi mwa Afrika

lakini mumewe akapelekwa katika mahakama ya ICC iliyoko The Hague.

Mahakama ya Ivory Coast imekataa katakata kwa wito uliotolewa na makundi mengine kuwa Simone Bgagbo apelekwe The Hague,

ambako mumewe anashtakiwa, yakidai kuwa mwanamke huyo na washtakiwa wenzake wanapaswa kukabiliana na makali ya sheria nyumbani.

Hadi kufikia leo alasiri Bi Gbagbo, mwenye umri wa miaka 65, hakuwa amefikishwa mahakamani.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja, wanasiasa, waandishi wa habari na wafuasi kadhaa wa Gbagbo

wamehojiwa mahakamani walipokuwa wakitoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao wanaoandamana na Bi Gbagbo.

Image caption Rais wa zamani Gbagbo akiwa mahakamani

Ingawa waandishi wa habari walilaumiwa mahakamani kuwa walichochea uhasama uliozusha ghasia nchini,

hakuna taarifa zo zote za habari wala kanda za sauti au video zilizowasilishwa mahakamani kuthibitisha kuwa walifanya hivyo.

Washtakiwa pamoja na wanasiasa kutoka upinzani wanadai kuwa mahakama itapendelea walioshinda

katika uchaguzi kwa sababu wanayo mamlaka juu ya taasisi zote za kutoa haki nchini.

Hakuna mtu yeyote aliye na uhusiano wa karibu na Ouattara aliyefanyiwa uchunguzi au kushtakiwa kuhusiana na ghasia hizo

zilizokumbwa mjii mkuu wa taifa kwa zaidi ya meizi mitano ingawa wengi wanafahamu kuwa upande wake pia ulichangia pakubwa ghasia zilizokumba taifa hilo.