Yanga yasonga mbele michuano ya Afrika

Image caption Wachezaji wa Yanga wakiwa na kocha wao Hans pluijm

Timu ya Young Africans maarufu kama Yanga ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobakia katika michuano ya Shirikisho la Kandanda barani Afrika, CAF kwa mwaka 2015.

Yanga wameweza kusonga mbele kwa kuwaondoa BDF XI ya Botswana kwa kuwacharaza jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijiji Dar es Salaam, Tanzania, wiki mbili zilizopita Yanga waliwafunga BDF XI magoli 2-0

Timu hizi ziliporudiana mjini Gaborone, Botswana, Ijumaa usiku, BDF XI waliibuka na ushindi wa magoli 2-1.

Hata hivyo ushindi huo haukuwasaidia kwani walijikuta wanatolewa katika mashindano kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2.

Sasa Yanga itacheza na timu ya FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua inayofuata. FC Platinum iliitoa Sofapaka ya Kenya.

Timu ya Azam iliyopata ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya El Mereikh ya Sudan, katika kinyang'anyiro cha klabu bingwa barani Afrika ilijikuta ikipoteza mchezo wa marudiano mjini Khartoum baada ya kulazwa mabao 3-0 na hivyo El Mereikh kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2.

Timu nyingine za Tanzania Zanzibar za KMKM na Polisi zimejikuta zikitupwa nje ya michuano ya vilabu barani Afrika kwa kupoteza michezo yao.