Uganda:Majeshi Afrika kuimarisha usalama

Image caption Mkuu wa Jeshi la Uganda Jenerali Katumba Wamala

Askari wa jeshi la Uganda wakishirikiana na wenzao kutoka mataifa mengine matano wameanza mazoezi ya kijeshi ikiwa mbinu za kupambana na kumaliza ugaidi chini ya kauli mbiu MALIZA UGAIDI. Mazoezi haya yanafanyika katika kambi ya Jinja kilomita Zaidi ya 80 mashariki mwa mji mkuu wa Kampala.

Washiriki wa mazoezi haya ya kijeshi yanahusisha Wanajeshi takriban 300 kutoka sio tu Uganda lakini pia Tanzania,Burundi, Uholanzi,Rwanda,na Marekani.

Akizindua rasmi zoezi hilo ambalo litaendelea hadi machi 14, mkuu wa jeshi la Uganda ,Jenerali Katumba Wamala amebaini kuwa linasaidia washiriki mbinu za kuwezesha kujitayarisha kusaidia operesheni za kulinda Amani, kusaidia utawala wa kiraia pamoja na kukabiliana na ugaidi.

Askari wa Marekani wanaongozwa na naibu kamanda wa kikosi cha Marekani barani Afrika-USARAF- Brigedia Generali Kenneth Moore Jr.amesema kuwa Uganda iko mstari wa mbele barani Afrika katika usuluhishi wa migogoro na pia kuwa mchangiaji mkubwa katika operesheni za kulinda Amani.

Uganda inashiriki katika operesheni za kulinda Amani nchini Somalia, na pia majeshi ya Uganda yanaisaidia kuimarisha ulinzi wa serikali ya Juba ya Salvar Kiir na pia ina vikosi nchini Jamhuri ya Afrika ya kati kama sehemu ya jeshi la Muungano wa Afrika katika juhudi za kuwasaka waasi wa kundi la Lord Resistance Army- la LRA.

Hii ikiwa ni fahari kwa utawala wa sasa wa Kampala kwa jeshi lake kushiriki katika operesheni nyingi nje ya nchi lakini wakosoaji hapa nchini na nje wanaulaumu utawala wa rais Museveni kwa kuingilia masuala ya nchi huru kwa madai ya kuimarisha usalama.

Nchi za Kenya, Ujerumani na Uingereza pamoja na mashirika kama vile ya chama cha msalaba mwekundu ,Umoja wa mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya hushiriki kama wachunguzi. Ushirika huu unaimarishwa wakati makundi ya kigaidi yanazidisha makucha yake katika kila pembe ya Afrika.

Mfano kundi la Boko haram limezidisha visa sio tu nchini Nigeria lakini pia katika nchi jirani za Cameroon na Tchad.Nchini Libya makundi yenye msimamo mkali yanajizatiti bila kusahau kundi la Al shabaab kujihami katika upembe wa Afrika na hivyo kutisha usalama wa mataifa ya Afrika mashariki.