Rais Kikwete:Mauaji ya Albino ni fedheha

Image caption Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete amekutana na Viongozi wa Chama cha Watu wenye Albino Tanzania na kuahidi kufanya kila liwezekanalo kuongeza nguvu ili kumaliza tatizo la amauaji ya dhidi ya Albino.

"Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo"alisema Rais.

Katika kikao hicho viongozi wa watu wenye Albino nchini wamesoma risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja ambayo itajumuisha Serikali, viongozi wa watu wenye Albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu katika suala hili ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini Tanzania.

Image caption Rais Kikwete akizungumza na wawakilishi kutoka Chama cha Albino Tanzania

Rais Kikwete amesema mauaji ya watu wenye Albino hayafanywi na Serikali bali watu ambao wako katika jamii zetu kwa kushirikiana na waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii hivyo ni lazima yakomeshwe.

"Kwenye familia, jamii na hatimaye vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo jukumu kubwa ambalo Serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa ushirikiano wa pamoja". Rais amesisitiza na kuongeza kuwa kamati hiyo ya pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya watu wenye Albino.

Rais Kikwete pia amesema Serikali itasaidia familia na wahanga wa vitendo vya mauaji kwa hali na mali ili waweze kujimudu na pia kuwapa ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo hivyo kwani vinawaletea waathirika na watu wanaoishi na Albino mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii na hivyo kushindwa kuendelea na maisha yao ama kufanya shughuli zao za kila siku.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jamii ya Albino imekuwa mashakani kutokana na vitendo vya mauaji vinavyosababishwa na imani za kishirikina

Katika kikao cha leo, viongozi wametoa kilio chao kwa serikali kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua kuwa zinatetea haki za watu wenye Albino nchini bado hazina mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.

Mapema leo asubuhi mara baada ya kufika Ikulu, kulitokea sintofahamu baina ya viongozi wa Chama cha Watu Wenye Albino na watu wasio wanachama kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi huo sio halali kwa vile muda wake umeshakwisha wa kukaa madarakani.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Albino, Ernest Kimaya ameelezea masikitiko kwake kwa Rais na kuelezea kuwa uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na wamemuomba Rais awasaidie kutimiza azma yao ya kuitisha mkutano na kuchagua viongozi wa Chama chao.

Kulingana na Bw. Kimaya wamepanga kufanya mkutano huo wa kuchagua viongozi katikati ya mwaka huu ambapo pia dunia itakua inaazimisha siku ya watu wenye Albino duniani.

Rais amekubali ombi hilo na hiyo itazungumzwa kwa urefu katika kamati ya pamoja ambayo inatarajiwa kuwa imekamilika wiki ijayo.