Chelsea yang'ang'ania kileleni EPL

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Chelsea wakifurahia ushindi katika mojawapo ya mechi zao za ligi kuu ya England

Ligi Kuu ya England hiyo ilitimua vumbi tena usiku wa kuamkia Alhamisi kwa viwanja saba kuumia nyasi ambapo vinara wa ligi hiyo, Chelesea imezidi kujizatiti kileleni.

Chelsea iliendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuibamiza West Ham bao 1-0, huku Manchester City ikiisasambua Leicester City kwa jumla ya magoli 2-0.

Nayo Manchester United ikajinyakulia pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle. Liverpool ikaibanjua Burnley mabao 2-0, Arsenal ikashinda ugenini mabao 2-1 dhidi ya QPR huku mashabiki wa Stoke City wakifurahia ushindi wa mabao 2-0 baada ya kuivuruga Everton.

Mchezo wa mwisho ulikuwa kati ya Tottenham dhidi ya Swansea, hadi mwisho wa mtanange huo wenyeji Tottenham wakawalaza wapinzani wao kwa ushindi wa mabao 3-2. Vinara wa ligi hiyo bado ni Chelsea yenye pointi 63 baada ya michezo 27, huku nafasi ya pili ikishikwa na Manchester City yenye pointi 58 baada ya kucheza mechi 28. Arsenal ipo nafasi ya tatu ikitia kibindoni pointi 54 wakitofautiana pointi moja na Manchester United inayoshikilia nafasi ya nne.

Mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo mpaka sasa kuna timu ya Leicester yenye pointi 18 baada ya michezo 27, juu yake ikitanguliwa na Burnley yenye pointi 22 sawa na QPR ambayo hata hivyo ina mchezo mmoja pungufu ya Burnley.