Pambano la watani wa jadi homa juu

Image caption Mashabiki wa Msimbazi, Simba

Kuelekea mechi ya ligi kuu nchini Tanzania kati ya watani wa jadi , homa imepamba moto na kwa hesabu za haraka haraka, mashabiki wapatao milioni 10 watakosa raha, ama kupata furaha kwa dakika 90 siku ya Jumapili wakati Simba na Yanga zitamenyana katika Uwanja wa Taifa (wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000), jijini Dar es Salaam.

Tayari majigambo yameanza na timu hizo mbili, moja ya timu kongwe barani Africa zikiwa na zaidi ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, zimeanza kambi maalumu kujiandaa na mechi hiyo muhimu, ambayo wakati mwengine hupelekea hata makocha kufukuzwa kazi, kwani ni kama mtaji wa uongozi.

Yanga, iliyoanzishwa mwaka 1935, tayari imefukuza makocha mara mbili, ambapo mwaka jana walimtupia virago kocha Mbrazil Marcio Maximo baada ya kufungwa na Simba 2-0 katika mechi isiyo ya ligi (Nani Mtani Jembe), na mwaka uliopita (2013), ilimtimua kocha Mholanzi Ernie Brandts, baada ya kufungwa na Simba 3-1 katika mechi nyingine ya Nani Mtani Jembe.

Hata hivyo, mara ya mwisho, katika mechi ya ligi kuu , timu hizo zilitoka sare 1-1, April 24 mwaka jana. Katika miaka ya nyuma ya hivi karibuni, Simba imeifunga Yanga zaidi ya mara nne, huku ushindi mnono ukiwa wa magoli 5-0 Mei 7, 2012 na kufanikiwa kutwaa ubingwa.

Tayari, kocha wa sasa wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic ametabiri mechi ya kukata na shoka, akiwaelezea Yanga kama kikosi kilicho vizuri msimu huu katika kugombania ubingwa na kwa sasa ikiongoza ligi ikiwa na pointi 31.

Kopunovic amesema anategemea kupata ushindi dhidi ya Yanga licha ya kuwa nafasi ya 5 katika msimamo (ikiwa na pointi 23), baada ya kusuasua kupata ushindi katika mechi kadhaa zilizopita na zile za mwanzo wa msimu wa ligi, ikiwa na rekodi ya kupata droo mfululizo katika mechi saba, ikiwa chini ya kocha aliyetupiwa virago, Mzambia Patrick Phiri.

Mhasimu wake, kocha Mdachi wa Yanga, Hans Pluijm, akilindwa na rekodi ya ushindi mfululizo katika mechi za ligi kuu na zile za michuano ya kombe la Vilabu barani Afrika, amesema kocha yeyote ana mategemeo ya ushindi, hivyo vijana wake, wana ari ya kushinda.

Mechi ya Simba na Yanga huvuta hisia za watu wengi nchini Tanzania na hupelekea baadhi ya mashabiki kuzimia uwanjani kutokana na presha, ama ya ushindi au kufungwa. Licha ya ligi kuu kuwa na timu 14, timu hizo mbili ndizo zinazoongoza kuwa ma mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.