Uzazi wakwamisha usawa makazini: ILO

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mwanamke mjamzito

Shirika la kazi duniani, ILO limesema miongo miwili tangu kufanyika kwa mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake huko Beijing, China, bado mustakhbali wa wanawake hususan sehemu ya kazi uko mashakani.

Katika taarifa yake kuhusu pengo la ujira wakati wa uzazi iliyotolewa kuelekea siku ya wanawake duniani, tarehe Nane Machi, ILO imesema masuala kama ajira na likizo ya uzazi kwa mama mzazi na mumewe inatekelezwa lakini bado kuna mengi ya kufanya.

Haki miliki ya picha MEHR
Image caption Mwanamke akiwajibika eneo lake la kazi

"Kuna adhabu ya makato ya mshahara kwa mwanamke mzazi ukilinganishwa na mwanamke asiye na watoto. Na hiyo ni nyongeza ya tofauti ya malipo kati ya wanaume na wanawake."

ILO imetolea mfano nchini Uingereza ambako mama anayelea mtoto anapata mshahara wenye pungufu ya asilimia 25 kuliko mwanamke asiye na mtoto, ilhali nchini Ujerumani tofauti ni asilimia 15.

Tofauti hiyo ni kando na ile ya jumla ambapo mshahara wa mwanamke ni asilimia 77 ya ule wa mwanaume huko Ujerumani.ILO inasema kama hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa, itachukua miaka 71 kwa wanawake kupata ujira sawa na wanaume.