Mama Maria Nyerere asema yuko hai

Image caption Mama Maria Nyerere asema yuko hai

''Niko salama na buheri wa afya''

Hayo ni maneno ya Mama Maria Nyerere ,mjane wa rais wa kwanza wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,alipojitokeza na kupinga uvumi uliokuwa ukienea kwamba ameaga dunia.

Madai kwamba Mama Maria alikuwa amefariki yalisambazwa katika mitandao ya kijamii siku ya jumatatu na kuzua wasiwasi katika taifa la Tanzania kabla ya kujitokeza na kukana madai hayo usiku katika runinga ya taifa.

Akizungumza na vyombo vya habari nyumbani kwake Masasani mjini Daresalaam, kwa zaidi ya saa moja ili kuonyesha kwamba yuko salama,amesema aligundua habari hizo kupitia mkaza mwanawe ambaye alimpigia simu

Alisema kuwa alipokea simu nyingi nyengine kutoka kwa familia ambao waliuliza kuhusu afya yake.

''lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na ushupavu wa kuniambia kuhusu uvumi wa kifo changu ambao ulikuwa ukienea katika mitandao ya kijamii.

''Kila mmoja aliyenipigia simu kabla ya mwanangu alisema kwamba alitaka kunisalimia'', alielezea akiongezea kwamba hakuwa na wasiwasi kwa kuwa yeye ni mcha mungu.

''Kwa kuwa mimi husali na kumuamini mungu,sikushangazwa na habari hiyo kwa kuwa hiyo ni kazi ya shetani ambaye ameshindwa'',alisema.