IS yatoa video ya mauaji ya 'jasusi'

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mussallam

Wapiganaji wa kundi la Islamic State wameweka kanda ya video katika mtandao ambayo inamuonyesha mvulana mdogo akimpiga risasi na kumuua mfungwa mmoja mwenye asili ya kiyahudi na kiarabu.

Mtu huyo anayejulikana kama Mohammed said Ismail Musallam anatuhumiwa na kundi la IS kwa kulifanyia kazi kundi la upelelezi la Israel Mossad.

Kijana huyo mwenye miaka 19 aliondoka nyumbani kwao mashariki mwa Jerusalem kwenda Uturuki mwaka uliopita ili kujiunga na kundi la IS nchini Syria.

Maafisa wa Israel na familia ya Mussallam zimekana kwamba alikuwa mpelelezi wa Israel.

Kanda hiyo ya Video haijathibitishwa na maafisa wa Israel wanasema kuwa hawawezi kuthibitisha chimbuko lake.

Familia ya Mussallam imesema kuwa alielekea nchini Uturuki miezi minne iliopita bila kuwaarifu.

Mda mfupi baada ya kuondoka kwake alimwambia nduguye kwamba alikuwa na mpango wa kujiunga na IS nchini Syria.

Msemaji wa shirika la usalama la Shin Beth ameliambia shirika la habari la AFP kwamba alikuwa amondoka nyumbani kwa kutaka kwake.

Familia ya Mussallam vilevile ilipokea simu kutoka kwa mtu ambaye alisema Mussallam alikamatwa katika kizuizi kimoja katika mpaka wa Uturuki na kuwekwa katika jela ya Islamic state.

''Hawakutaka aondoke kwa kuwa iwapo angeondoka na kurudi basi angekutakana na jeshi la Israel ambalo lingemtaka aelezee yote alioshuhudia''.Kwa hivyo walitaka kumuua'',Said Mussallam alinukuliwa na gazeti la Israel Yedioth Ahronoth. ''Namjua mwanagu nina hakika kwamba hakuwa akilifanyia kazi shirika la Mossad''.