Tanzania:Uchumi wa Raia Changamoto

Image caption Ufisadi waelezwa kuwakera Raia kiasi cha kutoiamini Serikali yao

Utafiti nchini Tanzania umebaini kuwa ukuaji wa uchumi hauna mchango katika maendeleo ya mtu wa kawaida na hivyo kuleta tafsiri tofauti kuhusiana na huduma za jamii zinazotolewa na serikali na watu kujenga chuki kwa serikali yao.

Shirika la utafiti nchini Tanzania REPOA katika ripoti ya utafiti wake kuhusu ukuaji uchumi,limesema kuwa pamoja na takwimu za ukuaji uchumi nchini Tanzania kuonyesha kuwa umekuwa kwa wastani wa asilimia 7 lakini bado kuna umasikini wa kipato kwa mtu

Lukasi Katera ni mtafiti kutoka shirika hilo la REPOA ameiambia BBC kuwa wamebaini kuwa baadhi ya viashria na matukio ya viongozi kuhusishwa na vitendo vya rushwa na hujuma ni mambo ambayo yanasababisha waichukie serikali yao na kuona hakuna kinachofanyika katika ukuaji wa uchumi.

Katera pia amesema kuwa matumizi yasiyo ya wazi ya fedha za umma ni viashiria vinavyowafanya wananchi kubeza kila jambo kuhusiana na suala zima la ukuaji wa uchumi na kutoridhishwa na huduma za jamii zinazotolewa na serikali yao.

Katika mapendekezo ya watafiti hao,ni kuimarishwa kwa sekta ya kilimo,kudhibiti kutokea kwa tuhuma za rushwa na kuhakikisha huduma za jamii zinaimarishwa hayo ni mambo yatakayorejesha Imani ya wananchi kwa serikali yao.

REPOA imekuwa ikijishughulisha kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi nchini Tanzania ambazo baadhi yake hutumika na serikali katika kutekeleza miradi na huduma za jamii.