Waandamaji 11 zaidi wakamatwa DRC

Haki miliki ya picha
Image caption Walikua wakihudhuria maandamano yaliyolenga kushinikiza serikali iwaachilie huru wanaharakati 20

Watu 11 wametiwa nguvuni mjini Goma mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo walipokua wakijiandaa kuandamana kupinga kukamatwa kwa wanaharakati, wanaounga mkono demokrasia katika mji mkuu wa kinshasa.

Duru zasema kuwa vikosi vya serikali viliwaumiza raia wawili wa Ubelgiji mmoja wao akiwa mtafiti.

Walikua wakihudhuria maandamano yaliyolenga kushinikiza serikali iwaachilie huru wanaharakati 20 kutoka Senegal, Burkina Faso na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waliokamatwa majuzi.

Kundi hilo linajumuisha raia wawili wa Ubelgiji, mtafiti mmoja na mwandishi mmoja wa habari ambao walikuwa wamefika hapo kuwasilisha malalamishi yao baada ya kudhulumiwa na maafisa wa polisi.

Mtafiti huyo angali anapokea matibabu katika hospitali moja mjini humo.

Image caption Watu 11 wamekamatwa nchini DRC

Kundi hilo lilikuwa likijiandaa kufanya maandamano dhidi ya kukamatwa kwa wanaharakati wa kidemokrasia na wasanii ambao walikamatwa pamoja na mfanyikazi mmoja wa shirika la maendeleo ya kimataifa ya Marekani USAID

na mwandishi mwengine wa kigeni siku ya Jumapili.

Mwandishi huyo wa habari wa kimataifa pamoja na afisa huyo wa kibalozi tayari wameachiliwa huru, lakini wanaharakati hao na wasanii wangali wanazuiliwa na maafisa wapolisi na ripoti zinasema kuwa wangali wanahojiwa.

Serikali ya congo imesema kuwa kundi hilo linashukiwa kupanga njama ya kuanzisha uasi nchini humo, lakini ubalozi wa marekani mjini kinshasa umesema kuwa wao walikuwa wakibadilishana mawazo kuhusu demokrasia.

Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Martin Kobler, amesema ameshangazwa na hatua hiyo ya serikali na kuwa ubalozi wa marekani na Ubelgiji wanafanya mazunguzmo na maafisa wa serikali ya Congo kujadili suala hilo.