Kimbunga Pam:Vanuatu wahitaji chakula

Haki miliki ya picha AP
Image caption Athari ya kimbunga Pam katika visiwa vya Vanuatu katika bahari ya Pasifiki

Umoja wa Mataifa katika visiwa vya Vanuatu umesema watu 24 wamekufa na wengine 3,300 hawana mahali pa kukaa baada ya kimbunga Pam kupinga visiwa hivyo vilivyo katika bahari ya Pasifiki mapema Jumamosi.

Timu ya Kupima majanga na Uratibu ya Umoja wa mataifa katika mji mkuu, Port Vila, imesema vituo 37 vya uokoaji vimeanzishwa, lakini mawasiliano na visiwa vingine bado ni tatizo.

Rais Baldwin Lonsdale amesema kimbunga hicho kimefutilia mbali maendeleo yote yaliyopatikana katika miaka ya karibuni.

Ametoa wito tena wa kuomba msaada wa kimataifa.

Kati ya waliokufa, 11 walikuwa wakitoka kisiwa cha Tafea, nane kutoka kisiwa kikuu cha Efate, na watano kutoka Tanna.

Vituo vya kutolea misaada vinawahudumia watu wengi waliopoteza nyumba zao, umesema Umoja wa Mataifa na kusema kuwa mwelekeo kwa sasa umeelekea katika mji mkuu na kisiwa kikuu cha Efate.

Baada ya ukaguzi uliofanyika kwa njia ya ndege kujua uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho, Shefa ni jimbo pekee lililotangazwa kuwa na hali ya dharura.

Misaada imeanza kuwasilishwa katika nchi hiyo iliyopigwa na kimbunga baada ya safari za ndege kurejeshwa katika mji mkuu Port Vila.

Vanuatu ni moja ya nchi maskini kuliko zote duniani.

Kimbunga cha Tropical Cyclone Pam taratibu kinapungua nguvu kikivuma kuelekea New Zealand na kinaonyesha kutokuwa na madhara zaidi kwa kisiwa cha Vanuatu au Pasifiki Kusini, imesema taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA).