Kenya na Uingereza kukabili ugaidi

Image caption Rais Kenyatta amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Markani Phillip Hammond

Uingereza imesema itasaidiana na Kenya katika kukabiliana na makundi ya kigaidi ili kuboresha amani kama njia bora ya kukuza uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Phillip Hammond amesema hayo baada ya Kenya na Uingereza kutia saini mkataba wa maelewano baina ya mashirika ya biashara na viwanda vya nchi hizo mbili.

Hamond amesema ukosefu wa usalama unatishia kuvuruga biashara kati ya nchi hizo mbili.

Wafanyabiashara wa Uingreza na Kenya wamepongeza kutiwa saini kwa mkataba wa kibiashara kati ya nchi zao.

Hafla hii iliongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Phillip Hammond na mwenzake wa Kenya Amina Mohamed.

Ijapokuwa utawala wa Uingereza kwa siku nyingi walikuwa wamejitenga na mahusiano ya moja kwa moja na serikali ya rais Kenyatta,

punde baada ya kuchaguliwa kwake mwaka 2013 kutokana na tuhuma za kuhusika na mauaji yaliyoikumba Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Kuwasili kwa Hamond nchini Kenya kuliashiria kuwa Uingereza imeanza kuukubali utawala wa Rais Kenyatta.

Image caption Marufuku kwa raiya wa Uingereza kuzuru Kenya kutokana na msururu mashambulizi ya kigaidi imeathiri utalii

Bwana Hamond alisisitiza kuwa biashara itafanikiwa tu chini ya mazingra bora ya usalama.

'' Tunafahamu vyema kuwa kwenye amani kuna mawasiliano na ushirikiano na pia biashara baina ya watu''alisema Hammond

Zaidi ya raia elfu ishirini na tano wa Uingereza wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kikazi na kibiashara nchini Kenya.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Kenya balozi Amina Mohamed alisema kuwa hatua ya Uingereza kuwapiga marufuku raia wao kuzuru Kenya kutokana na msururu wa mashambulizi ya kigaidi kumeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii.

Hatua hiyo ilisababisha mikahawa mingi kufungwa na wafanyakazi wengi wa hotelini walipoteza ajira kutokana na uhaba wa wageni.

''Kinachotuuma kwa hakika ni hatua ya serikali ya Uingereza kuendelea kutoa onyo kwa raia wake wasiingie Kenya ilhali hivi vita dhidi ya Ugaidi sio vyetu pekee'' alisema Amina.

Vivyo hivyo suala la Kenya kuandikisha mkataba mpya na Uingereza mkataba utakaowaruhusu wanajeshi wa Uingereza kuendelea kufanya mazoezi nchini Kenya lilijipenyeza katika ajenda.

Image caption Je Kenya itaweka mkataba mpya na Uingereza kuruhusu wanajeshi wa Uingereza kuendelea kufanya mazoezi nchini humo?

Balozi Amin Mohamed amesema '' mashauriano yanaendelea lakini uamuzi utakaochukuliwa utazingatia katiba ya Kenya na sheria za Uingereza''.

Hammond pia alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na kujadili masuala ya ushirikiano wa kibiashara na kidiplomasia kati ya Kenya na Uingereza.

Kabla na baada ya uchaguzi wa mwaka 2013 Serikali ya Uingereza ilikuwa imejitenga na Kenya wakati huo kesi ya jinai ikimkabli rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu, ICC.

Lakini Uingereza sasa imelegeza msimamo baada ya kesi iliyokuwa ikimkabili Rais Kenyatta kutupiliwa mbali kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hiyo.