Tunisia:Makavazi yafunguliwa leo

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hapo jana waziri mkuu wa taifa hilo aliwalaumu maafisa wakuu wa idara za usalama kwa kuzembea kazini

Makavazi ya Bardo nchini Tunisia, yanafunguliwa tena leo Jumanne, juma moja pekee baada ya magaidi kushambulia watalii wa kigeni na kuwauwa 20 kati yao.

Kutakuwa na mkutano wa hadhara kabla ya kufunguliwa tena kwa makavazi hayo ya kitaifa.

Wasanii watawatumbuiza wageni nje ya ukumbi huo unaopendwa na watalii wengi kutoka magharibi kabla ya maafisa kutoa taarifa inayolenga kuthibitisha kuwa magaidi hawataamua maisha ya wenyeji yasalie kuwa ya hofu.

Tangu tukio hilo kumekuwa na hofu kuwa magaidi hao huenda wameangamiza sekta nzima ya utalii ambayo ni kitega uchumi kikubwa cha Tunisia.

Hapo jana waziri mkuu wa taifa hilo aliwalaumu maafisa wakuu wa idara za usalama kwa kuzembea kazini .

Sita kati yao walitupwa nje.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa wa usalama wakishika doria nje ya makavazi hayo ya kitaifa

Waziri huyo mkuu , Habib Essid alisema mikakati imewekwa ilikuimarisha uwezo wa maafisa wa usalama kushirikiana na vitengo vya kijasusi kuzuia mashambulizi zaidi siku za usoni.

Jumba hilo linashehena kubwa zaidi ya sanamu za enzi za warumi.

Wavamizi wawili kati ya watatu waliotekeleza shambulizi hilo walipigwa risasi na kuuawa huku yule aliyesalia akisakwa na maafisa wa kitengo maalum cha kupambana na ugaidi.

Tukio hilo ndilo kubwa zaidi kuwahi kutokea baada ya mapinduzi ya kiongozi wa muda mrefu wa Tunisia Zine al-Abidine Ben Ali mwaka wa 2011.