Utah kuwapiga risasi waliohukumiwa kifo

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kiti kinachotumika kuua

Jimbo la Utah Nchini Marekani, limepitisha kubuniwa hukumu ya kupiga risasi na kuuwa, kwa wahalifu wote wanaohukumiwa kifo,

ikiwa dawa ya sumu ya kumdunga mhalifu haitapatikana.

Jimbo hilo la Utah limekuwa jimbo la pekee nchini Marekani kuanza kutumia mbinu hiyo ya hukumu ya kifo.

Ralph Dellapiana ni kinara mkuu wa kundi moja jimboni Utah, linalopinga aina yoyote ya hukumu ya kifo.

Gavana wa jimbo la Gary Herbert ambaye awali alionekana kupingana na njia hiyo ya unyongaji kwa sasa amekubali kutia saini ya kupitishwa kwa sheria hiyo kwa madai kuwa njia hiyo itakuwa mbadala pale dawa za sindano zinapo adimika.

Hata hivyo kwa wale ambao hawakubaliani na mbinu hiyo ya kunyonga watu waliohukumiwa kifo wanadai kuwa jimbo hilo linarejea mbinu ya kizamani na ambayo ilikwisha pitwa na wakati.

Dawa hizo kwa sasa zimeadimika nchini Marekani kwa kuwa zinatengenezwa ulaya ambako serikali zake zinapinga adhabu hiyo na kuiuzia Marekani dawa hizo za kunyongea.

Gavana Herbert amesema kuwa wakati umewadia kwa wadau wote kujadiliana na kutafuta mbinu mbadala .

Japo itachukua muda mrefu kabla ya watuhumiwa kunyongwa katika jimbo hilo,lakini upatikanaji wa madawa hayo ya kuwaua watu kwa sindano yanazidi kuwa nadra.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kituo kikuu cha kurekebishia tabia katika jimbo la Utah

Kwa sasa gavana huyo anasema kuwa jimbo hilo halina hifadhi ya dawa hizo za kunyonga.

Kufuatia shinikizo la umma jimbo la Utah limekatalia mbali ombi la wafungwa kuchagua mbinu itakayotumiwa kuwaua.

Hata hivyo kwa wale waliohukumiwa kunyongwa kabla ya mwaka wa 2004 watapewa fursa ya kuchagua wanataka kufa kwa njia ipi.

Ronnie Lee Gardner, ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuuawa kwa risasi yapata miaka mitano iliyopita.

Garner alikuwa amepatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumuua wakili mooja alipokuwa akijaribu kutoroka gerezani .