Ukanda wa Kati wapania kukuza uchumi

Image caption Injini ya treni ya mizigo ya kampuni ya Reli Tanzania, TRL

Marais wa Afrika Mashariki na kati wamezindua rasmi mradi wa mabehewa mapya ya mizigo yatakayokuwa yakisafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania kwenda katika nchi za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika eneo hilo.

Uzinduzi huo umefanyika Jumatano ambayo ni siku ya kwanza ya mkutano wa siku mbili unaotarajiwa kuhudhuriwa na marais wote wa nchi hizo, hata hivyo mpaka mkutano huo unaanza ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Pierre Nkurunzinza wa Burundi pamoja na mwenyeji wao Rais Jakaya Kikwete ndio waliokuwa wamehudhuria, huku Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakituma wawakilishi wao.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa nchi hizo na wawakilishi wa mashirika na taasisi za fedha na wawekezaji jijini Dar es Salaam, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema nchi yake imedhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za eneo la ukanda wa kati kwa kuboresha miundombinu ya barabara na reli na kupunguza kwa kiasi kikubwa urasimu katika utoaji wa huduma za bandari na vikwazo vya barabarani.

Haki miliki ya picha bb
Image caption Uzinduzi wa Treni ya Mizigo kwenda nchi za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutoka Dar es Salaam, Tanzania.

Tatizo la uchelewashaji mizigo katka bandari ya Dar es Salaam ni suala ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa na watumiaji wa bandari hiyo. Hata hivyo, sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi ambapo Katibu Mkuu wa wizara ya Uchukuzi nchini Tanzania Dakta Shaban Mwijaka amesema muda wa utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam umepungua kwa kiasi kikubwa kutoka siku 20 hadi siku tatu, sababu kubwa akisema ni matumizi ya mfumo wa kielektroniki badala ya kutumia makaratasi.

Nchi za Afrika mashariki na kati zimepiga hatua katika uimarishaji wa miundombinu ya barabara, hata hivyo rais Yoweri Museveni wa Uganda ameonya kwamba juhudi hizi hazitakuwa na tija iwapo juhudi zaidi hazitafanyika katika kuboresha miundombinu ya reli. Pia Rais Museveni amesema uvivu, rushwa na kutowajibika ni mambo yanayokwamisha ustawi wa maisha ya watu wa kawaida katika eneo hilo na Afrika kwa jumla.

Marais hao pia wamekagua miundombinu ya bandari, na kuitaka mamlaka ya bandari ya Dar es Salaam kuongeza ufanisi zaidi ili kuvutia wawekezaji katika sekta ya usafirishaji na miundombinu.