Mgahawa wa Kichina wakiri kuwazuia weusi

Haki miliki ya picha China Photos Getty Images
Image caption Raia wa Uchina wanakula mlo wa samaki

Wamiliki wa mgahawa wa kichina uliopo jijini Nairobi nchini Kenya ambao ulifungwa na mamlaka ya eneo hilo wamekiri kuwazuia watu weusi kuingia ndani baada ya saa kumi na moja jioni kwa kile alichokitaja kuwa maswala ya

kibiashara pamoja na ukosefu wa usalama usiku.

Wamesema kuwa waliidhinisha sheria hizo bila maonevu yoyote na kukiri kwamba sheria hizo hazikuwa sahihi na zilieleweka vibaya.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari wamiliki hao wanasema kuwa sheria hizo ziliwekwa baada ya wezi kuvamia eneo hilo na kutoweka na bidhaa fulani na kwamba hawakuwa wakimzuia mtu yeyote kuingia hoteli hiyo.

Mgahawa huo umekuwa ukigonga vichwa vya habari katika kipindi cha hivi karibuni kufuatia madai kwamba wakenya wanne walikatazwa kuingia kwa sababu walikuwa weusi.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Vyakula vya kichina vikitayarishwa katika hoteli ya raia wa Kichina

Usimamizi wa Hoteli hiyo hatahivyo umekana madai kwamba unawabagua raia weusi na kusema kuwa wamekuwa wakiwahudumia wateja wote bila kujali,kabila,rangi ama dini.

Maafisa wa polisi wamerekodi taarifa kutoka kwa usimamizi wa hoteli hiyo ambao unatarajiwa kushtakiwa kwa kuendesha biashara bila leseni halali.

Mbali na kutoa huduma za chakula,hoteli hiyo imekuwa ikitumiwa kama danguro kwa raia wa Uchina wanaoishi Nairobi.

Wakenya wameitaka serikali kufunga mgahawa huo na vilevile kuwashtaki wafanyibiashara hao kwa kueneza chuki na ubaguzi.

Hoteli hiyo inayosifika kwa mlo safi wa Kichina imefungwa kwa siku ya pili mfululizo.