Matumla kuvaana na Wang Xin Hua

Image caption Mabondia Xin Hua wa China na Mohamed Matumla wa Tanzania wakitambiana kabla ya pambano lao la Ijumaa

Bondia Mohamed Matumla wa Tanzania atapanda ulingoni Ijumaa kutwangana na Wang Xin Hua wa China.

Mchezo huu ni wa uzito wa super bantam kuwania nafasi ya kugombea taji la dunia la WBF utakaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam Tanzania.

Mshindi wa mpambano huu wa kukata na shoka atapata nafasi ya kupanda ulingoni kwenye mpambano wa utangulizi katika pambano litakalo wakutanisha wababe Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.

Hili litakuwa ni pambano la 17 kwa Mohamed Matumla, tangu aanze ngumi za kulipwa akiwa ameshinda mara 11, amepoteza mara 4 na kutoka sare mara 2.

Pambano hili litatanguliwa na mapambano kadhaa ya awali kati ya Ashraf Suleiman wa Tanzania ataonyeshana umwamba na Joseph Rabotte wa Marekani katika pambano la uzito wa juu.

Kalama Nyarawila na Thomas Mashali, wote wa Tanzania watapambana katika uzito wa kati kuwania taji la WBF.

Huku Japhet Kaseba wakipepetana na Maada Maugo katika uzito wa Light kuwania ubingwa wa taifa.