Taylor kukamilisha kifungo Uingereza

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor atakamilisha kifungo chake kilichosalia nchini Uingereza wala sio nchini Rwanda alivyotaka.

Aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor ameamrishwa na mahakama kutumikia kifungo chake kilichosalia nchini Uingereza baada ya kukataliwa ombi lake la kuhamishiwa nchini Rwanda.

Alitaka kuhamishiwa Rwanda kwasababu anadai kuwa ananyimwa fursa ya kupata haki yake ya kuwa karibu na familia.

Charles Taylor alighadhabishwa na kuwa mkewe na wanawe wamekataliwa vibali vya kusafiri Uingereza kuwa karibu naye.

Majaji wa kimataifa waliosikiliza kesi hiyo mjini the Hague hata hivyo wamekanusha madai hayo wakisema kuwa walinyimwa visa kwasababu whawakuweza kuwasilisha vibali vilivyotakiwa kisheria.

Katika uamuzi uliotolewa hadharani hii leo majaji hao wamesisitiza kuwa hatua ya Uingereza kuikatalia familia yake visa ya kuingia haikwenda kinyume na haki zao wala zake binafsi.

Mahakama hiyo pia imesema kuwa mkewe aliposhindwa kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika, pia alikataa usaidizi aliopewa na maafisa wa uhamiaji.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Charles Taylor alighadhabishwa na kuwa mkewe na wanawe wamekataliwa vibali vya kusafiri Uingereza kuwa karibu naye.

Mahakama hiyo inayoungwa mmkono na Umoja wa mataifa ilimkuta Taylor na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na hatua yake ya kuwaunga mkono waasi waliofanya maasi nchini Siera Leone.

Kesi yake Taylor ilisikizwa nchini The Hague Uholanzi na mahakama maalum iliyoteuliwa kusikiliza kesi ya Siera leone, lakini kwa masikizano kuwa hukumu yake Taylor itumikiwe nchi nyingine.

Uamuzi wa kusikiliza kesi hiyo nje ya Siera leone ulichukuliwa kwa hofu kuwa huenda kesi hiyo ingechochea ghasia zaidi nchini humo.

Taylor ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 67,na ambaye anatumikia kifungo cha miaka hamsini alipelekwa gereza la Frankland karibu na jimbo la Durham kaskazini mashariki mwa London mnamo October 2013.

Sierra Leone ilikumbwa na vita vibaya zaidi vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka wa 1991-2002.