Kwanini Buhari alimbwaga Goodluck ?

Haki miliki ya picha STATE HOUSE
Image caption Je kwanini wapiga kura wamemtema Jonathan ?

Raia wa Nigeria wameshazoea kuwa rais anayeongoza hawezikushindwa katika uchaguzi wa Nigeria!

Lakini leo Nigeria imefungua ukurasa mpya.

Rais aliyeko madarakani Goodluck Jonathan amesalia akijutia maamuzi yake baada ya raia wa taifa hilo kubwa zaidi Afrika kiuchumi kumpigia kura mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari .

Hizi hapa sababu 5 ambazo zinaelezea kwanini raia wa Nigeria walimng'oa Goodluck Jonathan mamlakani.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Haikuwa rahisi kuiba kura

1: Haikuwa rahisi kuiba kura

Katika Uchaguzi uliopita mwaka wa 2007 ,tuhuma za wizi wa kura za urais ziliibuka huku wadadisi na wachunguzi wakuu wakisema waziwazikuwa kura hazikuwa za huru wala haki.

Ripoti ya wachunguzi huru katika uchaguzi wa mwaka wa 2011 ilisema kuwa haukuwa wa uhuru japo ilisema kuwa idadi ya wizi ilikuwa imepungua mno.

Kufuatia ripoti hiyo tume huru ya uchaguzi nchini humo ilijiandaa na kuziba mianya iliyokuwa imebainika.

Tume hiyo ilinunua mashine za kuwasajili wapiga kura kwa njia ya kielektroniki na ving'amuzi vilivyotumika kubaini data ya mpiga kura.

Chama cha rais Goodluck Jonathan People's Democratic Party (PDP) kilikuwa kimepoteza ufuasi mkubwa katika majimbo yaliyokuwa ngome yake.

2 Boko Haram

Image caption Wapiganaji wa Boko Haram wamewaua watu 20,000

Uchaguzi huo umetangazwa huku raia wengi wa Nigeria wakikabiliwa na changamoto ya usalama wao haswa wakiwa mijini.

Hii inafwatia tishio la kundi la wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram ambao walikuwa wanaonekana ni kama wameishinda maarifa vyombo vya usalama wa kitaifa.

Boko Haram iliwaua zaidi ya watu elfu 20,000 na kuwalazimisha wenyeji zaidi ya milioni tatu kutoroka makwao.

Rais Jonathan hakuwa na jibu dhidi yao na alionekana mnyonge hadi majuzi majeshi ya muungano wa mataifa jirani yaliposhirikiana na jeshi la Nigeria na kuwavamia wanamgambo hao wa kiislamu.

Kura hizi zimefanyika zaidi ya majuma 6 baada ya kuahrishwa kufuatia tishio la kundi hilo lililokuwa limeapa kusambaratisha uchaguzi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Vyama tanzu vya upinzani vilijiunga chini ya muungano wa APC

3 Muungano wa Upinzani

Chama cha PDP kiliundwa kwa muungano wa viongozi kutoka matabaka ya kaskazini na vilevile kusini mwa taifa hilo.

Hata hivyo kufuatia utepetevu wa rais Jonathan viongozi wengi waliokuwa nguzo ya umoja huo walitawanyika.

Muungano wa viongozi wa upinzani chini ya nembo ya chama cha All Progressives Congress (APC)kuliwasaidia kukusanya kura zote katika kapu moja.

Kampeini za chama tawala zilikumbwa na madai ya hiyana na unafiki lakini vyama vya upinzani havikulegeza kamba .

Haki miliki ya picha
Image caption Uchumi mkubwa zaidi Afrika

4 Uchumi mkubwa zaidi Afrika

Ijapokuwa Nigeria inasifika kuwa taifa kubwa zaidi barani Afrika kiuchumi ,ukiwauliza raia wa Nigeria iwapo wamenufaika kwa njia yeyote ile watakuambia kuwa hawajanufaika kwa hali yeyote ile.

Takriban nusu ya raia wa nigeria wanaishi kwa hali duni ya uchochole na umaskini.

Wengi wao wanalaumu ufisadi wa viongozi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Uchumi wa Nigeria umekuwa kwa kiwango cha asilimia 5% kwa mwaka kutokana na mauzo ya mafuta lakini raia wengi hawakutaka kuendelea na utawala wa Goodluck.

Image caption Upinzani ulitumia kibwagizo ''Ni wakati wa Mabadiliko''

5 Ni wakati wa Mabadiliko

Wafuasi wa chama cha upinzani APC walichagua kibwagizo chao kikuu kuwa ''Mabadiliko''.

Na huenda wanigeria hawakuwa wanataka kuendelea na hali ilivyokuwa wakati huu.

PDP imekuwa madarakani tangu mwaka wa 1999, utawala wa kiimla ulipomalizika.

Mwaka huu 2015 Wapiga kura wameamua kumchagua kiongozi atakayekuwa na msimamo dhabiti na uwezo wa kukabiliana dhidi ya matatizo chungu nzima yanayowasakama

Hata hivyo kinachosubiriwa na wengi ni kuona iwapo rais Buhari ataleta mabadiliko kweli alivyowaagiza wapiga kura.