Ugaidi:Tanzania yajiweka katika tahadhari

Haki miliki ya picha MICHUZI BLOG
Image caption Maafisa wa polisi

Waziri wa Mambo ya ndani nchini Tanzania amesema nchi hio ipo katika tahadhari ya juu kufuatia taarifa za vyombo vya habari nchini humo kwamba, kuna uwezekano wa shambilio la ugaidi katika miji ya Dar es salaam na Mwanza.

Amesema hayo baada ya taarifa zilizo bainisha kuwa mmoja ya waliokamatwa katika shambulio la chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya ni Mtanzania.

Waziri wa mambo ya ndani , Matthais Chikawe, ameiambia BBC,mpaka sasa serikali ya Tanzania haijaweza kudhibitisha ripoti zinzaoenea ,kuhusu shambulio la ugaidi nchini humo.

Hata hivyo amesema vyombo vya dola nchi nzima viko macho na vimejitayarisha kwa lolote.

Pamoja na hayo waziri Chikawe amesema kuwa serikali ya Tanzania, inafahamu kuwa mmoja ya watuhumiwa walikokamatwa huko Garissa Kenya ni Mtanzania.

Hata hivyo amesema watawasiliana na polisi wa Kenya wakimaliza kumhoji mtuhumiwa huyo.

Tanzania ilikumbwa na shambulio la ugaidi mwaka 1998 wakati mabomu yalilipuka katika balozi za Marekani, jijini Dar es salaam na Nairobi, Kenya na kusabibisha vifo ya watu wengi.