Wito watolewa Congo ichunguze makaburi

Image caption Eneo lililozikwa miili mingi mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetakiwa kuchunguza miili ipatayo 421 iliyopatikana katika kaburi moja katika mji mkuu Kinshasa.

Harufu mbaya ndiyo iliyowaongoza wakazi wa eneo hilo mwezi Machi kufika katika sehemu iliyokuwa ikitoka harufu hiyo.

Serikali inasema miili yote ilizikwa usiku mmoja na ni pamoja na miili ya vichanga na miili ambayo ilikosa ndugu wa kuzika.

Lakini shirika la Human Rights Watch limesema inabidi waangalie iwapo kuna mtu yeyote aliyeuawa katika maandamano ya kuipinga serikali mwezi Januari alizikwa hapo.

Waandamanaji wengi waliuawa katika maandamano hayo ya kupinga mabadiliko ya sheria ya uchaguzi iliyokuwa inapendekezwa ikitaka ifanyike kwanza sensa ya kitaifa kabla ya uchaguzi wa rais kufanyika.

Shirika la Human Rights Watch, HWR lenye makao yake nchini Marekani limesema kuwa miili ya watu ilipotea wakati wa maandamano na pia wakati wa msako wa serikali dhidi ya magenge ya uhalifu mjini Kinshasa mwaka jana na mwaka 2013.

Wafanyakazi wa shirika la Human Rights,kwanza walipata fununu za eneo walipozikwa watu hao baada ya wakazi wa Maluku mjini Kinshasa kutoa taarifa ya kuwepo kwa harufu mbaya karibu na eneo la makaburi zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Mwanamke ammoja aliyekuwa akilima shambani aligundua mguu ukiwa umefukiwa chaini.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema kuwa miili hiyo ilizikwa kila moja na kaburi lake tarehe 19 Machi.

Msemaji wa serikali amesema Jumatatu kuwa hakutakuwa na kazi ya kufukua miili hiyo.