Rais Mugabe ziarani Afrika Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, anafanya ziara yake ya kwanza katika nchi jirani ya Afrika Kusini katika kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

Rais Mugabe aliwasili nchini Afrika Kusini Jumanne.

Ziara yake inakuja huku Zimbabwe ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na mgawanyiko ndani ya chama chake tawala cha ZANU-PF.

Waziri wa habari wa Zimbabwe Jonathan Moyo, ametupilia mbali taarifa kwamba ziara ya Bwana Mugabe nchini Afrika Kusini inalenga kuomba msaada.

Rais huyo wa Zimbabwe, ambaye ana umri wa miaka 91, ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU na Jumuia ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, SADC.

Wakati huo huo mwanachama wa ZANU PF aliyefukuzwa kutoka chama hicho tawala amesema chama kipya kitaundwa kumpa changamoto Rais Robert Mugabe.

Didymus Mutasa ameiambia BBC kuwa chama kipya pia kitaitwa Zanu lakini herufi PF itasimama badala ya maneno"People First" na siyo "Patriotic Front".

Zanu-PF ilimfukuza Bwana Mutasa na wanachama wengine waandamizi baada ya kuwatuhumu kupanga njama za kumtoa madarakani Bwana Mugabe mwaka uliopita. Wamekana madai hayo.

Bwana Mugabe, anatarajiwa kugombea tena kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Ameiongoza Zimbabwe tangu ipate uhuru wake mwaka 1980.

Bi Joice Mujuru msaidizi wa Bwana Mugabe aliyefukuzwa kutoka chama tawala cha ZANU PF , amedokezwa kuwa atakiongoza chama kipya kitakachoundwa.