UN yatakiwa kuondosha wakimbizi Kenya

Wakimbizi wa Somalia katika kambi ya Dadaab, Kenya Haki miliki ya picha Reuters

Serikali ya Kenya imeupa Umoja wa Mataifa miezi mitatu kuwahamisha wakimbizi wa Somalia kama nusu milioni na iwarejesha Somalia.

Makamo wa rais, William Ruto, alisema ikiwa Umoja wa Mataifa utashindwa kuwaondoa, basi Kenya yenyewe itafanya hivyo.

Amri hiyo imetolewa siku chache baada ya shambulio katika chuo kikuu kimoja cha Kenya lilofanywa na kundi la wapiganaji Waislamu wa Al Shabaab ambapo watu 148 waliuwawa.

Baadhi ya wakimbizi wa Somalia wamekuwa wakiishi katika kambi ya Dadaab mashariki mwa nchi kwa zaidi ya miongo miwili.

Siku za nyuma Kenya imewatuhumu Al Shabaab kuwa wanajificha kwenye makambi ya wakimbizi na kuajiri wafuasi wepya humo.