Urusi kuiondolea Iran vikwazo vya silaha

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov (R) wakisubiri mkutano wao nchini Uswis Machi 29,2015 kuzungumzia mpango wa nyuklia wa Iran

Marekani imepinga hatua ya Urusi ya kuiondolea vikwazo vya silaha Iran, huku Urusi ikilenga kuipatia nchi hiyo mfumo wa kudhibiti makombora ujulikanao kama S-300.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry alimpigia simu waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye amesema uamuzi wa hiyari uliochukuliwa na Urusi kuiwekea vikwazo vya silaha Iran mwaka 2010 hauhitajiki tena, kufuatia muundo wa makubaliano wa kimataifa wa mwezi uliopita kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia.

Marekani inachukulia vikwazo hivi kuwa sehemu ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa ambavyo havitakiwi kuondolewa hadi mwishoni mwa mwezi Juni wakati mkataba wa mwisho utakapofikiwa.

Waziri wa Ulinzi wa Iran, Hossein Dehghan amesema uamuzi wa Urusi utasaidia kuanzisha usalama na utulivu katika eneo hilo. Lakini Israel imekosoa hatua hiyo.

Waandishi wa habari wanasema Israel inahofia kuwa mfumo wa kudhibiti makombora wa S-300 utafanya mashambulio ya anga dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran kuwa magumu zaidi.