Wakimbizi:UNHCR yaahidi kushirikiana na Kenya

Image caption Shirika hilo limeitaka serikali ya Kenya kufikiria upya kauli hilo la kuwafurusha wakimbiz

Shirika la umoja wa mataifa linalosimamia wakimbizi UNHCR limesema kuwa liko tayari kufanya kazi na serikali ya Kenya ili kuhakikisha kuwa sheria za Kenya zinafuatwa kikamilifu katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab karibu na mpaka wake na Somalia.

Shirika hilo limeitaka serikali ya Kenya kufikiria upya kauli hilo la kuwafurusha wakimbizi na kufunga kambi hiyo katika kipindi cha miezi tatu ijayo.

Serikali ya Kenya ilitoa amri hiyo punde baada ya wanamgambo wa kiislamu wa Al Shabaab kuwaua wanafunzi wakristu takriban 150 katika chuo kikuu cha Garissa mapema mwezi huu.

Image caption Shirika linalosimamia wakimbizi UNHCR liko tayari kushirikiana na Kenya kukomesha utovu wa usalama katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab

Makamu wa Rais William Ruto alitangaza kuwa angetaka wakimbizi hao warejeshwe makwao na kambi hiyo ya Dadaab ifungwe.

Kambi hiyo yenye wakimbizi takriban nusu milioni ndio kubwa zaidi duniani ikiwa na asilimia kubwa ya wakimbizi kutoka Somalia.

Serikali ya Kenya imesema inaushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa asilimia kubwa ya mashambulizi yanayotekelezwa nchini Kenya na kundi la waislamu la Al Shabaab yanapangiwa katika kambi hiyo ya Dadaab.

Haswa ikiashiria shambulizi la maduka ya kifahari ya Westgate ambapo ilidaia washambulizi waliingia nchini kama wakimbizi.

UNHCR inapinga madai hayo.

Image caption Kenya imedai kuwa Al Shabaab inapanga mashambulizi katika kambi hizo za wakimbizi

UNHCR inasema kuwa Kenya itakuwa inakiuka wajibu wake wa kuhakikishia wakimbizi usalama wao pindi wapoingia katika mipaka yake.

Serikali ya kenya kwa ushirikiano na UNHCR na serikali ya Somali iliweka mipango ya kurejesha wakimbizi makwao mwaka uliopita lakini mkataba huo ulikuwa utekelezwe kwa hiari.

Idadi ndogo sana ya wakimbizi hao walikubali kurejea makwao.