Mama aliyeua Watoto Marekani ahukumiwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Megan Huntsman, Mwanamke aliyehukumiwa kifungo kwa mauaji

Mwanamke mmoja katika Jimbo la Utah nchini Marekani ambaye alikiri kuua watoto wake wachanga sita wa kuzaa mwenyewe huenda akahukumiwa Kifungo cha maisha gerezani.

Megan Huntsman, 40, alikamatwa mwaka mmoja uliopita baada ya miili ya Watoto kukutwa kwenye maboksi katika gereji ya Nyumba yake ya zamani.

Mwezi Februari alikutwa na hatia kwa makosa sita ya mauaji.

Jaji wa mjini Provo alitoa hukumu dhidi ya mwanamke huyo ya takriban miaka 30 mpaka kifungo cha maisha.

Polisi wamesema Watoto hao walizaliwa kati ya mwaka 1996 na 2006 na kueleza hali ya Watoto hao kuwa mauti iliwakuta kwa kukosa hewa au kwa kukabwa na Huntsman mara tu baada ya kuzaliwa.

Polisi wamesema miili aliiweka kwenye mifuko ya plastiki na kuiweka kwenye maboksi.

Mwanamke huyo aliacha maboksi hayo katika Nyumba aliyoishi alipokuwa akihama, miili iligunduliwa na mumewe,Darren West, mwezi Aprili mwaka jana.Mtoto wa saba pia anaaminika alipoteza maisha wakati mwanamke huyo alipokuwa akijifungua.

Polisi wanasema Huntsman alikuwa akitumia dawa zenye nguvu ziitwazo methamphetamine, dawa zinazosisimua neva mwilini ili kuwezesha akili na mwili kufanya kazi kwa uchangamfu, pia mwanamama huyo hakuwataka Watoto hao.

Maafisa wanasema West ni Baba wa Watoto lakini yeye si mshukiwa wa tukio hilo.Yeye na Huntsman wana Watoto watatu.

Mwezi Aprili mwaka 2014 West aliachiwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka minane gerezani kwa makosa ya kujihusisha na uhalifu wa madawa, hivyo alikwenda kwenye nyumba kwa ajili ya kukusanya vitu vyake ndipo alipogundua miili ya Watoto.

Uamuzi wa mwisho kuhusu muda ataotumikia Huntsman gerezani uko mikononi mwa jopo la wanasheria.Waendesha mashtaka wamesema huenda akatumikia kifungo cha maisha.