Kuacha mashambulizi ni hatua nzuri:IRAN

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ndege ya jeshi la Saudi Arabia ikipaa kwenda kushambulia Yemen

Iran imeutaja uamuzi wa Saudi Arabia wa kusitisha mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, kuwa hatua iliyo nzuri.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Java Zarif , alisema kuwa hatua hiyo inastahili kufuatiwa na mazungumzo pamoja na msaada wa dharura wa kibinadamu.

Msemaji wa muunganmo unaoongozwa na Saudi Arabia, alisema kuwa kwa sasa lengo ni kupatikana kwa suluhu la kisiasa kwa mzozo ulio nchini Yemen, lakini hata hivyo hakusema ikiwa nguvu za kijeshi hazitatumika.

Rais Abdrabbuh Mansour Hadi wa Yemen ambaye alikimbilia usalama wake nchini Saudi Arabia aliishukuru nchi hiyo kwa msaada wake.

Lakini licha ya mashambulizi ya mwezi mzima, bado bwana Hadi amesalia kuishi uhamishoni huku waasi wa Houthi bado wakiudhibiti mji mkuu Sanaa.