Mama na mwanawe waagizwa kurudi London

Image caption Mahakama ya Uingereza

Waziri wa maswala ndani nchini Uingereza ametakiwa kumrudisha mwanamke mmoja na mwanawe wanaotafuta hifadhi nchini humo miezi kadhaa tu baada ya kuagiza aondolewe, mahakama ya rufaa imeamuru.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 45 na mwanawe walirudishwa nchini Nigeria mnamo mwezi Januari.

Mwezi uliopita mahakama ya uhamiaji ilisema kuwa Theresa May hakuangazia maslahi muhimu ya kijana huyo mwenye umri wa miaka mitano.

Wakati huohuo ndege iliotarajiwa kuwasafirisha watafutaji hifadhi 59 iliahirisha safari yake hadi nchini Afghanistan baada ya agizo la mahakama la dakika za mwisho.

Rufaa ya wakili wa Bi May dhidi ya hatua hiyo ya mahakama ya uhamiaji katika kesi ya mwanamke huyo na mwanawe ilikataliwa na Jaji McCombe.

Alisema kuwa haiwezekani kuamua kwamba hatua hiyo ilikuwa ya makosa.

Mahakama ya rufaa iliambiwa mjini London kwamba mpango wa kuwasafirisha wawili hao kurudi mjini London siku ya Alhamisi ulikuwa umewekwa.

Mwanamke huyo raia wa Nigeria alikamatwa akifanya kazi katika duka moja kinyume na sheria nchini Uingereza akitumia pasipoti ya uongo ya Uholanzi mwaka 2007.

Aliwasilisha ombi la kuishi London na kusema amekuwa katika taifa hilo tangu mwaka 1991,lakini ombi lake likatupiliwa mbali.

Mwanamke huyo baadaye alitaka uhifadhi mwaka 2010,akisema kuwa alihofia mateso iwapo angerudi nchini Nigeria,ni wakati huo ambapo alikuwa amejifungua mwanawe.

Lakini jopo la uhamiaji liliamuru mwezi uliopita kwamba waziri wa maswala ya ndani nchini Uingereza alifeli kuangazia athari za kiafya zilizomkabili mamaake na hatari zake iwapo angerudishwa nchini Nigeria.