Tutafuzu michuano ya Mataifa ya Afrika.

Image caption Rais wa TFF,Jamal Malinzi

Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF) limesema limeweka malengo kuhakikisha timu ya taifa ya vijana ya U17 inafuzu kucheza fainali za Mataifa Afrika 2017 nchini Madagscar, na baadae kuwa na kikosi bora wakati Tanzania inapojiandaa kuwa wenyeji wa fainali za U17 Afrika mwaka 2019.

Raisi wa TFF , Jamal Malinzi amesema shirikisho lake lina program mbili za kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 13, 15 kwa kuwaweka kambini na kucheza michezo ya kirafiki mikoani na kufanya ziara katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Bostwana na Afrika Kusini.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kozi ya makocha jijini Dar es Salaam, Malinzi amewaomba walimu wakufunzi kuwa karibu na makocha wa timu za Taifa, na kuwapa ushauri makocha hao ili kuweza kuwasaidia katika kuboresha vikosi vyao na maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.

Naye Rais wa Baraza la Vyama vya Soka katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati (CECAFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) , Leodgar Tenga alimshukuru Malinzi kwa kuweza kufungua kozi hiyo ambayo inawakutansisha walimu wakufunzi wa mpira wa miguu kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Walimu hao watatumika kuandaa timu mbalimbali na kuzalisha vijana wenye vipaji kwa ajili ya kucheza timu za taifa.

Kozi hiyo, itakayomalizika Mei 2 mwaka huu, inawajumuisha walimu 18, wenye leseni A, B na C za CAF kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar