Burundi: Wanafunzi watahadharishwa

Haki miliki ya picha
Image caption hali ya usalama ni tete nchini Burundi, watu watano wameripotiwa kupoteza maisha

Wanafunzi katika chuo kikuu cha Burundi mjini Bujumbura, wanasema kuwa serikali imewaagiza kufungasha virago vyao na kuondoka chuoni hapo mara moja kwani chuo hicho kinafungwa.

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na maandamano yaliyokumbwa na ghasia ambazo bado zinaendelea nchini humo kutokana na hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza atawania Urais kwa muhula mwingine wa tatu.

Watu watano wameripotiwa kufariki tangu kuzuka kwa ghasia hizo siku kadhaa zilizopita.

Umoja wa mataifa umeonya kuwa huenda taifa hilo likaingia katika lindi la mzozo wa kisiasa, iwapo ghasia hizo zitakithiri, mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo mwezi Juni.

Maafisa wakuu wa umoja wa mataifa na mwanadiplomasia wa Marekani, kwa sasa wanashauriana na serikali ya Burundi, ili kukabiliana na taharuki hiyo ya kisiasa.

Mapema polisi walitibua maandamano ya watu waliokuwa na lengo la kuweka vizuizi kwa raia Nkurunzinza kuwasilisha stakabadhi zake hii leo kama mgombea wa urais wa nchi hiyo.