Rais Nkurunziza asema uchaguzi ni lazima

Image caption Raia wa Burundi wakiwa mtaani

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, amepuuzia wito uliotolewa na nchi ya Marekani pamoja na umoja wa Ulaya juu ya wito uliotolewa kuhusu uchaguzi uahirishwe.

Rais Nkurunziza ameiambia BBC kwamba kuahirishwa kwa uchaguzi kutaliingiza taifa hilo katika mgogoro mkubwa zaidi."unapoona asilimia tisini na tisa ya nchi yote ina amani na usalama hii ina maana mazingira yanaruhusu uchaguzi kufanyika .

Unaweza kusema kwamba uchaguzi usitishwe ikiwa watu wote wanazungumza lugha hiyo ya kusitishwa kwa uchaguzi ,na hiyo itakuwa na maana kwamba tutakuwa na serikali ya mpito.

Hatuwezi kukubaliana na wito huo hata kidogo hapa nchini Burundi,kwasababu kukubaliana na wito huo ni kukaribisha vurugu kubwa zaidi na matatizo makubwa zaidi mbeleni hasa tukiunda serikali ya mpito."

mpaka sasa watu tisa wamepoteza maisha yao katika vurugu zilizo dumu kwa wiki ya pili sasa ,vurugu zenye lengo la kukinza maamuzi ya rais wa nchi hiyo Nkurunziza asigombee nafasi ya urais kwa muhula wa tatu.

Kufuatia vifo hivyo rais Nkurunziza amesema kwamba anasikitika kutokana na vifo hivyo,na kwamba vurugu hizo zimesababishwa na kile anacho kielezea kama ushawishi kutoka mataifa mengine:

"kwa kawaida unapozungumzia juu ya suala la maandamano sio suala la kwenda kuua watu wala kuwashambulia polisi na hata kuchoma moto magari na kadhalika.

Ina maana kwamba yakitukia mabo kama hayo wakati wa maandamano basi hayo siyo maandamano,hiyo ni sawa na vita,ndiyo maana tunasikitika kutokana na vifo vilivyotokea wakati wa maandamano hayo lakini ni lazima tuwe na maamuzi ya kusitisha vurugu na hivyo basi kuwaruhusu watu kuingia kwenye harakati za uchaguzi."