Mwandishi auawa Bangladesh

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ananta Bijoy alishambuliwa mtaani alipokuwa akitembea kwenda kazini

Mwandishi wa blogu asiyefungamana na masuala ya dini nchini Bangladesh ameuawa kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana kaskazini mashariki mwa Bangladesh katika mfululizo wa matukio matatu ya watu kuuawa kwa kushambuliwa tangu kuanza mwaka huu.

Polisi wamesema Ananta Bijoy Das alishambuliwa na kundi la watu walioficha sura zao wakiwa wamebeba mapanga katika mji wa Sylhet.

Bwana Das aliandika katika blogu ya Mukto-Mona, ukurasa wa mtandao ambao awali ulisimamiwa na Avijit Roy, ambaye naye aliuawa kwa kukatwa mwezi Februari.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Avijit Roy alikua msimamizi wa Blog ambayo Ananta alifanya kazi.Avijit aliuawa mwezi Februari

Bwana Roy, mwandishi wa Marekani mzaliwa wa Bangladeshi, alikosoa kwa kushindwa kuvumiliana kutokana na imani ya kidini.

Aliuawa kwa kushambuliwa na mapanga wakati akizuru mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, akirejea na mkewe kutoka maonyesho ya vitabu mjini humo.

Mjane wake alipata majeraha ya kichwa na kupoteza kidole gumba.

Image caption Mke wa Avijit Roy alikatwa kidole wakati wa Shambulio la mwezi Februari

Mwezi Machi, mwandishi mwingine wa blogu, Washiqur Rahman, aliuawa kwa kuchinjwa mjini Dhaka.

Sara Hossain, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu mjini Dhaka, ameiambia BBC kuwa Bwana Das na Bwana Roy walikuwa katika orodha ya watu wanaolengwa na mashambulio hayo.

"Daima waliamini na kuandika kwa ukali wakiunga mkono uhuru wa kujieleza na walijibainisha katika maandishi kwa wenyewe kutofungamana na dini yoyote," ameiambia BBC.

"Waandishi wawili wamekuwa sehemu ya blogu iitwayo Mukto-Mona (Free Mind) au Mawazo Huru, ambayo ni kuwa fikra za kujitegemea na ilikuwa katika kushughulikia itikadi kali za kidini na hususan msimamo mkali wa dini ya Kiislam. Majina yao yalikuwa yameorodheshwa katika mashambulio."

Shambulio la mwezi uliopita kuhusu Bwana Roy liliibua maandamano makubwa kutoka kwa wanafunzi na wanaharakati wa kijamii, ambao wameishutumu serikali kwa kushindwa kuwalinda watu wanaokosoa misimamo ya kidini.

Mwiislam mmoja amekamtwa kuhusiana na mauaji ya Bwana ROY, wakati ambapo wanafunzi wawili wa madrassa wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Bwana Rahman.