Prince Charles kukutana na Gerry Adams

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Prince Charles wa Uingereza

Mwana wa Mfalme wa Uingereza Prince Charles anatarajiwa kukutana na rais wa Sinn Féin, Gerry Adams mwanzoni mwa ziara yake nchini Ireland Jumanne.

Bwana Adams atakuwa miongoni mwa wanasiasa watakaomlaki Prince Charles atakapoanza ziara yake ya siku nne.

Kukutana kwao huko Galway itakuwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya Ireland kati ya uongozi wa Sinn Féin na mwana familia wa Familia ya Kifalme ya Uingereza.

Mwenyekiti wa chama Declan Kearney amesema ni kukuza uelewano na kuponya makovu ya mambo yaliyopita.

Bwana Kearney amesema Gerry Adams na Martin McGuinness watakutana na mwana mfalme.

"Hii ilikubaliwa kukuza mchakato wa kutatua uonevu uliopita na kukuza uelewano na kusameheana," amesema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gerry Adams kiongozi wa Sinn Fein

Mwaka 2012, Bwana McGuinness alikutana na Malkia huko Belfast kutokana na wadhifa wake kamanaibu waziri wa kwanza wa Ireland Kaskazini.

Kushikana mkono kati ya Malkia Elizabeth na kamanda wa zamani wa IRA, katika ukumbi wa Lyric Theatre huko Belfast, ilichukuliwa kuwa tendo la kihistoria.

Wakati wa ziara yake Charles, akiandamana na Duchess wa Cornwall, atatembelea kijiji cha Mullaghmore katika kaunti ya Sligo - ambako baba yake mkubwa, Earl Mountbatten, aliuawa kwa bomu la IRA mwaka1979.