Burundi:Nkurunziza ahairisha uchaguzi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Burundi:Nkurunziza ahairisha uchaguzi

Rais wa Burundia Pierre Nkurunziza amehairisha uchaguzi wa wabunge kwa siku kumi .

Msemaji wa rais Willy Nyamitwe ameiambia shirika la habari la AFP kuwa kufuatia jaribio la mapinduzi juma lililopita na vurugu zilizofuatia ni bora kuahirisha uchaguzi huo kwa muda.

''Uchaguzi huo wa ubunge ulikuwa umeratibiwa kufanyika tarehe 26 mwezi Mei lakini sasa inatubidi kuhairisha ili kuwasikiza washirika wetu wa kimataifa pamoja na tume ya uchaguzi ambayo pia inatumia muda huo kutatua maswali yaliyoulizwa na vyama vya upinzani.'' alisema Nyamitwe.

Hadi kufikia sasa tarehe rasmi ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanywa Juni tarehe 26 haijabadilika.

''Subiri tu'' Nyamitwe aliwaambia waandishi wa habari.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi waaminifu kwa Nkurunziza walizima jaribio la mapinduzi juma lililopita

Mwandishi wa BBC aliyeko huko Ruth Nesoba amesema kuwa tayari rais Nkurunziza ametia sahihi amri hiyo ya kuhairishwa kwa uchaguzi.

Umoja wa mataifa ya bara Ulaya EU, na Umoja wa mataifa ya Afrika AU, yametoa wito kwa uchaguzi huo uliokumbwa na utata mkubwa uhairishwe ilikutoa fursa kwa mazungumzo ya upatanishi kuendelea .

Hapo jana Rais wa Afrika Kusini alitilia pondo hoja hiyo ya kuahirisha uchaguzi akisema ni bora uchaguzi huo uliopangwa ''uahirishwe''.

Takriban watu 20 wameuawa kufuatia makabiliano baina ya polisi na waandamani katika mji mkuu wa Bujumbura kilele ikiwa ni juma lililopita makamanda waasi walipotangaza jaribio la mapinduzi rais

Nkurunziza akiwa mjini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kanda uliolenga kutatua mzozo wa kisiasa nchini mwake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji wamekuwa wakipinga kauli ya Nkurunziza ya kutaka kuwania muhula wa tatu

Wapinzani wa rais Nkurunziza wanasema kuwa kutangazwa kwake nia ya kuwania muhula wa tatu unakiuka sheria na makubaliano ya amani ya mwaka wa 2006 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13.

Nkurunzizakwa upande wake anashikilia kukutu kuwa ana haki ya kuwania muhula mwengine kwani muhula wa kwanza hakuchaguliwa na wanainchi bali wabunge.

Takriban watu laki moja wamekimbilia mataifa jirani wakihofia kutibuka upya kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.