Je Korea Kaskazini inamiliki zana za Nuklia ?

Haki miliki ya picha EPA KCNA
Image caption Je Korea Kaskazini inamiliki zana za Nuklia ?

Korea Kaskazini imesema kuwa inaendelea kuimarisha mipango yake ya kupunguza ukubwa wa zana zake za kinyukilia.

Shirika Kuu la habari nchini humo limesema kuwa taifa hilo haliwezi kutishwa na taifa lingine lolote juu ya uimarishaji wake wa zana za kivita.

Tangazo hilo limetolewa muda mfupi baada ya Pyongyang kuzuia ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon nchini humo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Haijulikani iwapo Korea Kaskazini imefaulu kuweka zana hizo kwenye kombora au la

Shirika la habari la taifa lilisema kuwa taifa hilo limepiga hatua kubwa katika juhudi zake za kufanya zana zake za kinukilia kuwa ndogo na zenye uwezo wa kutumiwa kwenye makombora.

Hata hivyo haijulikani kwa hakika kama taarifa hiyo ilimaanisha kuwa imefaulu kutengeneza zana ndogo inayoweza kuwekwa kwenye kombora au la.

Tangazo hilo linafuata kuchapishwa kwa picha zinazoonyesha kombora likifyatuliwa kutoka kwa nyambizi, ingawa wataalamu wa picha kutoka nje ya nchi wanasema kuna ishara kuwa picha hizo zimechapishwa kwa njia ya kuvuruga ukweli.

Ukweli uliopo ni kwamba Korea Kaskazini imeanza kujigamba sana kwa sasa, ingawa hakuna ushahidi wa kuthibitisha iwapo kujigamba huko kuna mashiko au la.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Pyongyang imemzuia Katibu Mkuu wa UN Ban Ki Moon kuzuru viwanda vya Kaesong.

Katibu Mkuu wa Umoja Umoja wa Mataifa, Ban-Ki Moon, aliyetarajiwa kutembelea Korea Kaskazini kesho sasa hataweza kufanya hivyo baada ya Serikali ya Pyongyang kumnyima ruhusa ya kuzuru ukanda wa mitambo ya kuzalisha bidhaa mbalimbali nchini humo.

Moon amesikitishwa mno na hatua hiyo ya kumnyima ruhusa dakika za mwisho mwisho kabla ya ziara.

Wakati huohuo msemaji wa idara ya ulinzi ya Korea Kusini Kim Min-seok ameitaka utawala wa Korea Kaskazini kukomesha mpango wake wa kuzalisha zana za kinyuklia.