Palmyra yaitekwa na ISIS

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wapiganaji wa Islamic State

Wapiganaji wa Islamic State wameuteka mji wa kale wa Palmyra nchini Syria kutoka majeshi yanayoiunga mkono serikali ya nchi hiyo.Televisheni ya serikali ya Syria inasema wapiganaji hao wa Islamic State wanajaribu kuingia katika mji huo wa kale kuelekea kusini mwa mji huo.

Mji huo muhimu kimkakati unaunganisha maeneo ya mashariki na magharibi ya nchi na unawawezesha wapiganaji kuwa karibu zaidi na mji mkuu wa Syria Damascus. Televisheni ya serikali ya Syria imesema majeshi yameondoka kutoka eneo hilo na wakazi wengi wa mji huo wameondolewa. Kuna hofu kwamba wapiganaji hao wataharibu mabaki ya kale ya miaka elfu mbili iliyopita, kama walivyofanya katika maeneo mengi ya kale. Mkuu wa makumbusho nchini Syria amesema mamia ya vitu vya thamani vya kale vimehamishwa kutoka eneo la Palmyra, lakini majengo ya minara ya enzi ya Kirumi hayawezi kuhamishika. Kwa upande wake mkuu wa Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, ameelezea kusikitishwa na hali hiyo.

Omar Hamza ni mwanafunzi wa zamani wa masomo ya biashara ambaye bado anaishi katika mji huo na anaeleza kuwa kwa sasa ni mwanaharakati. Ameiambia BBC kuwa eneo hilo limetekwa na wapiganaji wa Islamic State."Utawala huu umepoteza udhibiti wa hospitali kubwa magharibi mwa mji. Islamic State wameitwaa hospitali hiyo na maeneo mengi ya magharibi. Islamic State pia wameteka kabisa eneo la kaskazini la Palmyra. Mapigano ni makali kati ya wapiganaji wa Islamic State na majeshi ya serikali. Huwezi kumwona mtu yeyote katika mitaa. Lakini wengi wa raia hawana mahali pa kujihifadhi kwa hiyo wanatumia majengo ya shule kama nyumba za kuishi. Kuna walenga shabaha wa serikali wakiwa juu ya majengo mengi na kuwepo kwa ndege nyingi za kivita." Anasema Omar Hamza.

Wapiganaji wa IS wamekuwa wakiendesha harakati zao katika nchi za Syria na Iraq ambapo hivi karibuni wameripotiwa kuuteka mji wa Ramadi nchini Iraq, ambako majeshi ya nchi hiyo wakipambana vikali na wapiganaji hao.