Ufaransa: Tumeua wanamgambo wawili Mali

Haki miliki ya picha
Image caption Mamia ya wanajeshi wa Ufaransa wapo nchini Mali kama sehemu ya juhudi za kupambana na ugaidi.

Vikosi maalum kutoka Ufaransa vimewaua wapiganaji wanne wa kijihadi, wakiwemo viongozi wawili katika shambulizi eneo la kaskazini mwa Mali. Haya ni kwa mujibu wa wizara ya ulinzi nchini Ufaransa.

Mmoja wa wale waliouwawa ni Amada Ag Hama, anyeshukiwa kuhusika katika utekajinyara na mauaji ya wanahabari wawili wa Ufaransa mwaka 2013.

Anasemekana kuwa kamanda wa al-Qaeda katika eneo lenye Waislamu wengi la Maghreb.

Ufaransa iliwatuma wanajeshi wake nchini Mali miaka miwili iliyopita wakati wanamgambo wa kiislamu walipotishia kuuteka mji mkuu, Bamako. Wanajeshi 3,000 wa kikosi cha ufaransa bado wapo katika eneo hilo kukabiliana na ugaidi.

Kiongozi mwingine aliyeuwawa ametajwa kwa jina la Ibrahim Ag Inawalen, kutoka kundi jingine lenye ufungamano na al-Qaeda, Ansar Dine.

Mbali na mauaji ya waandhishi wa Radio ya kimataifa ya Ufaransa, RFI, Ghislaine Dupont na Claude Verlon, Amada Ag Hama pia alihusishwa na kifo cha mfanyikazi wa shirika la kutoa misaada Michel Germaneau na katika utekajinyara wa raia wanne wa ufaransa nchini Niger, wote mwaka 2010.

"Ufaransa ina kumbukumbu ndefu,'' amesema waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Laurent Fabius.

Mali ilikumbwa na mapinduzi mwaka 2012. Na kisha vurugu zilipotokea, waasi wa kabila la Tuareg walichukuwa udhibiti wa eneo la kaskazini na kutangaza uhuru wao, kabla ya kupokonywa na kisha kutimuliwa na wanamgambo wa Kiislamu.

Hali bado ni tete katika eneo hilo, licha ya Ufaransa kuingilia kati na uwepo wa wanajeshi alfu kumi na moja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaojulikana kama Minusma.

Siku ya jumatano, mshambuliaji alifyatulia risasi makao ya Umoja wa Mataifa mjini Bamako na kumjeruhi bawabu.