FIFA:Blatter ailaumu UEFA na Marekani

Haki miliki ya picha PA
Image caption Blatter ailaumu UEFA na Marekani kwa kuendesha kampeini ya chuki dhidi ya FIFA

Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter ameikashifu shirikisho la soka barani ulaya UEFA na Marekani kwa kuendesha kampeini ya kuipaka tope jina zuri la FIFA.

Blatter ambaye ameanza muhula wake wa tano kama rais wa shirikisho hilo amesema kuwa alipigwa na mshangao alipopata habari za ufisadi ulaji na rushwa ndani ya FIFA.

Akizungumza na runinga moja ya Uswisi Blatter alimtaja mkuu wa sheria wa Marekani Loretta Lynch na rais wa UEFA Michel Platini kwa kuichukia FIFA.

''Kwa kweli chuki inayosikika katika tuhuma za ufisadi na ulaji rushwa dhidi ya FIFA kwa hakika sio kitu cha kudhaniwa na mtu mmoja hiyo ni chuki ya shirikisho lote la UEFA.

''Lakini mimi nitawasamehe tu '' alisema Blatter.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa FIFA Sepp Blatter ,na mpinzani wake Ali Bin al Hussein mwanamfale wa Jordan

Blatter alilaumu vyombo vya habari kwa kujaribu kuchochea njama ya kuiharibia FIFA jina.

Blatter alitawazwa rais wa FIFA baada ya kujiondoa kwa mpinzani wake Ali Bin al Hussein mwanamfale wa Jordan baada ya kushindwa katika mkondo wa kwanza wa uchaguzi kwa kura 133 kwa 73.

Blatter, ambaye ameongoza shirikisho hilo kwa miaka 17 amewataka wajumbe wa FIFA kushirikiana na kuwa imara. .

Akifungua mkutano mkuu wa FIFA mjini Zurich, Bwana Mr Blatter alibainisha kuwa shirikisho hilo linakabiliwa na matatizo - lakini akatoa wito kwa wajumbe kushughulikia matatizo hayo kwa pamoja.

Lakini kabla upigaji kura , mpinzani mkuu wa bwana Blatter , Ali Bin al Hussein mwanamfale wa Jordan, aliwaomba wajumbe wa mkutano huo kumuunga mkono -- kwa ajili ya kuboresha mchezo wa soka

Ali Bin al Hussein mwanamfale wa Jordan alijiondoa kabla ya kupigwa kura ya mkondo wa pili.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wajumbe katika kongamano la FIFA

Blatter alikuwa akiungwa mkono na mashirikisho ya soka ya afrika Asia na Marekani Kusini huku Ali Bin al Hussein mwanamfale wa Jordanakiungwa mkono na UEFA.

Wakati huohuo,wafadhili wakuu wa shiriko la kandanda duniani FIFA wanasema kuwa wanatarajia raisi wake aliyechaguliwa kwa mara nyingine Sepp Blatter kuchukua hatua madhubuti ili kurejesha hadhi ya shirikisho hilo iliyochafuka.

Kampuni za Coca-Cola na McDonalds zimeitaka FIFA kuchukua hatua za haraka kwa munufaa ya mchezo wa soka na mashabiki kote duniani.

Bwana Blatter alichaguliwa tena kwa muhula wa tano siku ya ijumaa licha ya kuwepo uchunguzi unaofanywa na Marekani na Uswisi kuhusu kashfa zinazolikumba shirikisho hilo za ufisadi na ulaji rushwa dhidi ya maafisa wake wakuu.