Viera awania umeneja Newcastle United

Image caption Patrick Viera anayewania nafasi ya kuwa kocha mkuu wa Newcastle United ya England

Mchezaji kiungo wa zamani wa Arsenal na Manchester City Patrick Vieira yuko katika orodha ya watu wanne waliochujwa kushika nafasi ya kocha wa timu ya Newcastle United.

Steve McClaren, ambaye alitupiwa virago na timu ya Derby County wiki iliyopita, naye yumo katika orodha hiyo.

Mchakato wa mahojiano utaanza wiki hii kwa Vierra mwenye umri wa miaka 38 kuhojiwa. Kocha huyo wa timu ya Manchester City kwa wachezaji chini ya umri wa miaka 21 amejiandaa kukabiliana na mikimiki ya ligi kuu.

Vieira, ambaye alikuwa katika kikosi cha timu ya Ufaransa iliyotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998, aliwahi kushinda pia mataji matatu ya ligi na makombe manne ya FA katika miaka yake tisa akiwa na timu ya Arsenal.

Alihamia Juventus ya Italia mwaka 2005 lakini alirejea katika ligi kuu ya England mwaka 2010 alipojiunga na Manchester City na kuisaidia kushinda kombe la FA mwaka 2011 kabla ya kustaafu soka miezi miwili baadaye.

Iwapo atafanikiwa atakuwa miongoni mwa makocha wanne vijana kuliko wote katika orodha ya makocha wa sasa wanaofundisha katika ligi kuu ya England.

Newcastle imekuwa haina kocha mkuu wa kudumu tangu Alan Pardew ajiunge na Crystal Palace mwishoni mwa mwaka jana.

Newcastle, ambayo ilimaliza nafasi ya 15 katika msimu wa 2014-15 wa Ligi Kuu, inatumaini kumteua meneja wake katika kipindi cha wiki mbili zijazo.