Ghana yaanza kwa kishindo AFCON

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachezaji wa timu ya Ghana wakishangilia kwa pamoja.

Kindumbwendumbwe kwa mataifa ya Afrika kufuzu kucheza fainali za Afcon mwaka 2017 kimeanza kwa michezo kadha kuchezwa mwishoni mwa wiki.

Ghana ilikuwa na kazi nyepesi baada ya kuirarua Mauritius magoli 7-1.

Asamoah Gyan na Jordan Ayew wote walifunga mara mbili wakati Ghana ikiilaza Mauritius kwa mabao 7-1.

Ghana ilifungwa na Ivory Coast kwa penalti katika fainali za mwaka huu, lakini sasa inaonekana kupania kucheza fainali za mwaka 2017.Mchezo huo wa kundi H ulichezwa mjini Accra, Jumapili.

Ghana iliwazidi kwa ubora Mauritius ambayo imewahi kucheza mara moja katika historia ya michuano hiyo ikiwa ni mwaka 1974.

Nayo Nigeria ikiikaribisha Chad mjini Kaduna iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku Afrika Kusini ikishindwa kuutumia vema uwanja wao baada ya kutoka suluhu ya 0-0 na Gambia.

Kwa timu za Afrika Mashariki Uganda ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana, Rwanda ikiilaza Msumbiji bao 1-0, huku Kenya ikitoka sare ya bao 1-1 na Congo. Burundi imecharazwa na Senegal mabao 3-1, nayo Tanzania ikiambulia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Misri.