England yaichabanga Slovenia 3-2

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Timu ya England wenye jezi nyekundu wakipambana na Slovenia mjini Ljublijana. England ilishinda 3-2

Timu ya taifa ya England imezidi kujiimarisha katika kusaka nafasi ya kucheza fainali za Ulaya mwaka 2016 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Slovenia.

Slovenia ndio waliokuwa wa kwanza kutikisa nyavu za England katika dakika ya 37 likifungwa na Milivoje Novakovic.

Hata hivyo Jack Wilshere aliweza kufunga mabao mawili katika dakika ya 57 na 73 ambapo Slovenia walisawazishisha kupitia kwa Nejc Petnik katika dakika ya 84.

Dakika mbili baadaye nahodha wa timu ya England Wayne Rooney aliweza kuipatia timu yake ushindi kwa kupachika bao katika dakika ya 86.

England imezidi kuongoza kundi E lenye timu za Estonia, San Marino, Lithuania, Switzerland na Slovenia.

Baadhi ya michezo iliyochezwa Jumapili ni pamoja na ule kati ya Sweden na Montenegro ambapo Sweeden iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Hispania ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Belarus. Austria iliicharaza Urusi bao 1-0, nayo Uswisi ikiibwaga Lithuania kwa mabao 2-1 na Ukraine ikiigaragaza Luxembourg mabao 3-0.

Katika michezo ya Jumamosi Ujerumani iliifanyia mauaji Gilbratar kwa kuitandika magoli 7-0 nayo Poland ikiilaza Georgia mabao 4-0 huku Scotland na Jamhuri ya Ireland zitoka sare ya bao 1-1.