Blazer ndiye aliyedukua mikutano ya FIFA

Haki miliki ya picha AP
Image caption Blazer ndiye aliyedukua mikutano ya FIFA

Aliyekuwa afisa wa kamati kuu ya shirikisho la soka duniani FIFA amegunduliwa kuwa ndiye aliyekuwa akidukua mawasiliano ya wanakamati wenza kwa kipindi cha miezi 18 katika jitihada za kujinasua kutoka kwa tuhuma za ulaji rushwa ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka dhidi yake.

Chuck Blazer mwenye umri wa miaka 70 anadaiwa kuungana na wapelelezi wa idara ya upelelezi ya Marekani FBI kuchunguza kisiri FIFA kati ya 1997-2013.

Makubaliano hayo yalifichuliwa baada ya jaji kuitikia ombi la mashirika matano ya uandishi wa habari.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa 14 wa FIFA wameshtakiwa kwa kupokea hongo na ufisadi

Barua hiyo inaonyesha kuwa Blazer alikuwa akishirkiana na FBI kisiri tangu Disemba 2011.

Mwezi uliopita, waendesha mashtaka wa Marekani aliamuru kukamatwa kwa maafisa 14 wa FIFA kwa mashtaka ya ulanguzi wa pesa, na ufisadi iliyohusu zaidi ya dola milioni mia moja.

Mkataba huo wenye kurasa 19 ulitiwa saini Novemba mwaka wa 2013 siku ambayo Blazer alikiri makosa yake lakini inaonyesha makubaliano yaliyosainiwa kati yake na serikali ya Marekani yalitiwa sahihi Disemba 2011.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Blazer alikuwa na kalamu aliyotumia kudukua mikutano ya FIFA kisiri kati ya 1997-2013.

Barua hiyo inasema "mshtakiwa anakubali kushirikiana na afisi ya mpelelezi nyaraka zote na vifaa vingine vinavyohitajika katika uchunguzi huu.''

''Ushirikiano huu na shughuli zote za kisiri zitakazotekelezwa kulingana na masharti ya maafisa wa upelelezi na makubaliano ya idara ya sheria."

Jarida la New York Daily lilieleza mwaka uliopita kuwa Blazer alidukua mikutano ya maafisa wakuu wa FIFA kwenye mashindano ya Olimpiki 2012 kupitia waya ya kisiri iliyofichwa kwenye kalamu.