Mlipuko wa bomu wawaua watu 23 Nigeria

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bomu Nigeria

Watu 23 wameuawa Kaskazini mwa Nigeria wakati mabomu yaliyokuwa yameachwa nyuma na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram yalipolipuka katika kambi yao ya zamani.

Wapiganaji wa kiraia wanaosaidiana na Serikali kupambana na Boko Haram walikuwa wakipekua kambi hiyo iliyokuwa imehamwa na wapiganaji wa Boko Haram karibu na mji wa Monguno wakati milipuko ilipotokea.

Inadaiwa kuwa watu hao walikuwa wakisherehekea baada ya kupata mabomu hayo wakati ambapo bomu moja lililipuka na kusababisha madhara hayo makubwa.

Tukio hilo linaonyesha baadhi ya matatizo ambayo raia wanaendelea kukabiliana nayo hata wakati Boko Haram wanapoendelea kutimuliwa.