Pagan Amum arejeshwa serikalini S Kusini

Haki miliki ya picha
Image caption Pagan Amum

Katibu mkuu wa chama tawala nchini Sudan kusini amerudishwa katika wadhifa wake baada ya kuishi kwa mwaka uhamsihoni nchini Kenya.

Pagan Amum alitimuliwa kwenye chama cha SPLM pamoja na kundi la wanasiasa wanaompinga rais Salva Kiir.

Mgogoro kati ya serikali na kundi pinzani ulizua ghasia ambazo zimawalazimu zaidi ya watu milioni moja kutoroka makaazi yaomnamo mwezi Disemba mwaka 2013.

Tangazo hilo lilifanywa baada ya mkutano wa maafisa wa vyeo vya juu katika SPLM leo katika mji mkuu wa Juba.

Msemaji wa Chama Akol Paul alisema kuwa kumrejesha kazini Pagan Amum ni kwa manufaa ya amani na utangamano.

Alisema kuwa huu ulikuwa ni mwisho wa kundi lijulikanalo kama "G10" akigusia kundi la wakimbizi wa kisiasa, akiwemo bwana Amum, waliotorokea taifa jirani la Kenya.

Kundi hilo linatarajiwa kukutana na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar katika juhudi za kuangamiza mzozo wa kisiasa unaoendelea Sudan Kusini.

Rais Salva Kiir alimsimamisha kazi bwana Amum mwaka 2013 baada ya madai ya utovu wa nidhamu na kisha akamfukuza kazini kabisa.